Na SUZANE CHEDDY
15th January 2015
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willbrod Slaa.
Alidai kwamba aliamini mkewe, Josephine Mushumbuzi, angeweza kumtambua kwa haraka mtumiaji wa simu namba (0754 013237) anayejiita Jaji Samatta kwa kuwa mkewe ni mtaalam mbobezi wa Teknolojia ya Mawasiliano ya Kompyuta na aliweza kumjua mtu huyo baada ya kumtumia mhamala wa Sh. 500 kwa njia ya M-Pesa.
Jaji Samatta feki, anadaiwa alitumia jina hilo kutafuta nauli ya kwenda Dar es Salaam kuzungumza na Dk. Slaa ili aisaidie Chadema ishinde kesi ya Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, ya kuvuliwa ubunge wake kupitia rufaa namba 47 ya mwaka 2012 iliyofunguliwa na Lema dhidi ya Mussa Hamis Nkanga na wenzake. Lema alikuwa akipinga hukumu ya Mahakama Kuu ya Arusha kumvua ubunge.
“Mke wangu alinipa mrejesho baada ya kutuma Shilingi 500 kwa njia ya M-Pesa kwenda namba (0754 013237) na akanitaarifu kwamba namba hiyo imesajiliwa kwa jila la Abeid Abeid na siyo Barnabas Samatta. Nikaamua kumtumia (Abeid anayejiita Jaji Samatta) ujumbe mfupi wa maneno (sms) kwa kutumia simu yangu (0783 967519) Mr. Abeid the game is over, naamini kwamba upo mzima. (yaani bwana Abeid, mchezo umekwisha),” alidai.
Dk. Slaa alidai kwamba muda huo huo, Abeid anayejiita Jaji Samatta, alimjibu kwa kumtumia ujumbe mfupi, “Nimeamini chama chenu (Chadema), ni chama kinachofuata haki bila ya kununua. Natangaza kuwaunga mkono kuanzia leo. Na akajitambulisha mwisho wa ujumbe huo kwamba yeye ni Afisa wa Takukuru, Wilaya ya Ulanga, lakini kwa sasa yupo Arusha.
Mshitakiwa huyo, (Abeid Abeid) anakabiliwa na kesi ya jinai namba 117 ya mwaka 2013 ya jaribio la kumtapeli Dk. Slaa, akitumia jina la Jaji Mkuu Mstaafu, Barnabas Samatta kujipatia fedha.
Mwendesha Mashitaka wa Takukuru mkoa wa Kilimanjaro, Susan Kimaro, aliyekuwa akisaidiwa na wakili Furahini Kibanga,, alimtaka Dk. Slaa kuieleza mahakama hiyo kama aliwahi kuzungumza na Jaji Samatta ambaye si aliyeko mahakamani hapo, na Slaa akaieleza mahakama kwamba alizungumza naye baada ya Jaji, Thomas Mihayo, kumpatia namba halali ya Jaji Mkuu mstaafu (Samatta.
“Nilimtafuta siku hiyo hiyo, lakini hakupatikana na asubuhi ya Aprili 12 mwaka 2012, Jaji Samatta halisi na si huyu feki ninayemuona hapa, alinipigia simu akaniambia hajawahi kufanya mawasilino na Godbless Lema wala Profesa Abdallah Safari ambaye wakati huo alikuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema. Alishtuka sana nilipomueleza kuna kesi kama hiyo ya yeye kutaka apewe fedha za nauli ili aje Dar es Salaam kusaidia kutoa mbinu ili Lema ashinde kesi yake iliyopo Mahakama ya Rufaa,” alidai Dk. Slaa.
Slaa aliendelea kudai kwamba baada ya kumjibu Samatta feki ujumbe huo, alimtumia ujumbe mwingine unaosema: “Baba nakushukuru sana, lakini kwa sababu namna namna misingi ya Chadema ilivyo; hatuwezi kufanya kitu hicho, lakini pia Lema amefungua kesi
namba 47 ya mwaka 2012 katika Mahakama ya Rufaa.”
Alidai kuwa baada ya kumueleza Jaji Samatta kuhusu sakata hilo, alimjibu kwamba muelekeo wa hayo mawasiliano kati ya Samatta feki na yeye (Dk. Slaa) yanaakisi kwamba Chadema nayo, inataka kuingia kwenye mkumbo wa rushwa na kumshauri kufanya kazi ya kuvisaidia vyombo vya dola kuanza kuchunguza mawasiliano hayo.
CHANZO ;NIPASHE
No comments:
Post a Comment