15th January 2015
Mkurugenzi wa Huduma ya Sheria wa Wizara ya
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Rugonzibwa Mujunangoma (kulia) na
picha ya kushoto, Mhandisi wa Mamlaka ya Umeme Vijijini (Rea),Theophillo
Bwakea, wakifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es
Salaam jana kujibu mashtaka ya rushwa baada ya kudaiwa kupokea mgao wa
fedha zinazohusiana na akaunti ya Tegeta Escrow. P
Katika kesi ya kwanza, aliyekuwa Mwanasheria wa Mamlaka ya Vizazi na Vifo (Rita), Mujunangoma ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa Wizara Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, alisomewa mashtaka yake mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Emmilius Mchauru.
Upande wa Jamhuri ukiongozwa na Mwendesha Mashitaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai, akisaidiana na Max Ari, ulidai kuwa Februari 5, mwaka jana katika Benki ya Mkombozi iliyopo Ilala jijini Dar es Salaam, mshtakiwa huyo akiwa Mkuu wa Sheria wa Wizara hiyo, alipokea rushwa.
Ilidaiwa kuwa mshtakiwa huyo alipokea rushwa ya Sh. milioni 323.4 kama zawadi kupitia akaunti yake namba 00120102062001 kutoka Rugemalira ambaye ni Mshauri wa kimataifa binafsi na Mkurugenzi wa zamani wa IPTL baada ya kuwa mjumbe katika manejimenti ya Rita wakati wa machakato wa kuipitisha IPTL kuliuzia Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) umeme.
Ilidaiwa kuwa mshtakiwa huyo alipokea kiasi hicho cha fedha kama zawadi hiyo akiwa ofisa wa muda wa kushughulikia masuala ya IPTL.
Mshtakiwa huyo alikana mashtaka.
Swai alidai upande wa Jamhuri hauna pingamizi la dhamana kwa mshtakiwa huyo, hivyo mahakama ijielekeze katika hati ya mashtaka ya fedha anazodaiwa kuchotewa mshtakiwa huyo kutoka kwenye akaunti hiyo ya Tegeta Escrow.
Hakimu Mchauru alisema mshtakiwa huyo atakuwa nje kwa dhamana endapo atatimiza mashrti kwa kujidhamini kwa fedha taslimu Sh. milioni 160 au hati ya mali isiyohamishika yenye thamani kiasi hicho cha fedha.
Vilevile alisema awe na wadhamini wawili wanaofanyakazi serikalini, watakaosaini hati ya dhamana ya Sh. milioni 10 kila mmoja na mshtakiwa asitoke nje ya Dar es Salaam bila kibali cha mahakama hiyo.
Mshtakiwa huyo alitimiza baadhi ya masharti ya dhamana, hivyo Hakimu huyo kumpa muda wa kukamilisha hati za mali zake na kuziwasilisha keshi (Ijumaa) mahakamani hapo kuhakikiwa.
Katika kesi ya pili; aliyekuwa Mjumbe wa Kitengo cha kuidhinisha Tanesco kununua umeme wa IPTL katika Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Bwakea ambaye kwa sasa Mtumishi wa Wakala wa Umeme Vijijini (Rea), alisomewa mashitaka yake mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Frank Moshi.
Swai alidai kuwa Februari 12, mwaka jana mshtakiwa huyo akiwa Mhandisi Mkuu wa Rea, alipokea rushwa ya Sh. milioni 161.7 kupitia akaunti namba 00410102643901 kutoka kwa Rugemalira ikiwa ni mgao wake kutoka kwenye akaunti ya Tegeta Escrow kama zawadi.
Ilidaiwa kuwa mshtakiwa huyo alipokea kiasi hicho cha fedha baada ya kuwa mjumbe aliyeandaa sera zinazohusu sekta binafsi kuzalisha na kuuza umeme kwa Tanesco.
Mshtakiwa huyo naye alikana mashtaka yake.
Upande wa Jamhuri ulidai hauna pingamizi la dhamana na kwamba upelelezi dhidi yake umekamilika.
Hakimu Moshi alimtaka mshtakiwa huyo kuwa na wadhamini wawili kutoka serikalini au wanaofanyakazi katika taasisi zinazotambulika watakaosaini hati ya dhamana ya Sh. Milioni 20 kila mmoja.
Pia alisema mshtakiwa huyo hatakiwi kutoka nje ya Dar es Salaam bila kibali cha mahakama.
Mshtakiwa aliachiwa baada ya kutimiza masharti ya dhamana na kesi yake kuahiridhwa hadi Januari 26, mwaka huu itakapotajwa tena.
Jana majira ya saa 2:00 asubuhi, wafanyakazi na watu mbalimbali waliingia kwenye viunga vya mahakama hiyo, huku kukiwa na minong’ono kuwa wanaotuhumiwa ufisadi wa Escrow watafikishwa mahakamani hapo.
Pia waandishi wa habari waligawanyika katika makundi tofauti huku wakijadili na kutafatuta wadau wao kujua kuhusu ujio wa watuhumiwa hao.
Saa 5:42 asubuhi washtakiwa hao walitinga mahakamani hapo na kwenda kusomewa mashitaka yao yanayowakabili.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment